Tuesday, November 23, 2010

KWA NINI CCM ILISHINDWA IRINGA MJINI


OKTOBA 31, mwaka huu, ulifanyika uchaguzi mkuu  wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini kote. Katika uchaguzi huo, CCM iliibuka na ushindi katika maeneo mengi hivyo kuendelea kupata ridhaa ya kuongoza nchi.

Katika mkoa wa Iringa, uchaguzi ulifanyika katika majimbo yote 11, ambapo Rais Jakaya Kikwete aliibuka mshindi katika kura za urais dhidi ya wagombea Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), Peter Mziray (APPT Maendeleo), Profesa Ibrahim Lupimba (CUF), Fahmi Dovutwa (UPDP), Hashim Rungwe (NCCR Mageuzi) na Mugahywa Muttamwega wa TLP.

Rais Kikwete, majimbo  na kura alizopata kwenye mabano ni Iringa Mjini (18,457), Ismani (18,541), Kilolo (42,112), Ludewa (24,523), Kalenga (29,532), Mufindi Kusini (28,596), Njombe Kaskazini (30,240), Njombe Magharibi (32,283), Njombe Kusini (30,024), Mufindi Kaskazini (30,752) na Makete 19,642.

Kwa upande wa ubunge, CCM iliingia katika uchaguzi huo ikiwa na Wabunge watano kibindoni ambao walikuwa wamepita bila kupingwa. Wabunge hao ni Mahamoud Mgimwa (Mufundi Kaskazini), Menrad Kigola (Mufindi Kusini), Deo Filikunjombe (Ludewa), anne Makinda (Njombe Kusini) na William Lukuvi (Ismani).

Kutokana na hali hiyo, ilikuwa na imani kwamba ingezoa majimbo yote yaliyobaki hivyo kuendeleza rekodi ambayo imejiwekea tangu mwaka 2000 ya kuwa na wabunge wote kutoka Chama tawala.

Tangu kuanza kwa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, CCM ilipoteza ubunge katika jimbo la Iringa Mjini baada ya aliyekuwa mgombea wake, Dk. Hassy Kitine, kubwagwa na Mwalimu Mfwalamagoha Kibassa wa NCCR Mageuzi.

Rekodi hiyo imewekwa tena mwaka huu kwa kupoteza jimbo hilo baada ya aliyekuwa mbunge wake, Monica Mbega, kuangushwa na Mchungaji Peter Msigwa wa CHADEMA. Monica ambaye ndiye aliyelikomboa jimbo hilo kutoka NCCR Mageuzi mwaka 2000, aliangushwa kwa kupata kura 16,916 dhidi ya 17,748 za Mchungaji Msigwa.

Kwa majimbo mengine ya Kilolo, Kalenga, Njombe Magharibi, Njombe Kaskazini na Ludewa yaliyokuwa na wagombea kutoka vyama vingine, wagombea wa CCM waliibuka kidedea ama kwa kutetea nafasi zao au kwa kushinda kwa mara ya kwanza.

Waliotetea nafasi zao ni Profesa Peter Msolla wa Kilolo na Dk. Binilith Mahenge wa Makete. Injinia Gerson Lwenge (Njombe Magharibi) na Deo Sanga (Njombe Kaskazini), walishinda kwa mara ya kwanza baada ya kupitishwa na CCM. Majimbo hayo yalikuwa yakishikiliwa na Jackson Makwetta na Yono Kevela am,bao waliangushwa katika kura za maoni.

Hata hivyo, katika majimbo ya Njombe Magharibi na Kaskazini, kulikuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wagombea wa CHADEMA, Thomas Nyimbo na Alatanga Nyagawa. Wagombea hao wa CHADEMA walikuwa wana CCM kabla ya kujiunga na chama hicho kufuatia kuenguliwa au kusindwa katika kura za maoni.

Kutokana na kujiengua CCM, walisababisha upinzani mkali kwani baadhi ya wafuasi wao ambao ni wanachama wa CCM walikuwa wakiwaunga mkono. Hatua hiyo iliifanya CCM kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha  inashinda katika uchaguzi huo.

Licha ya kuungwa mkono na baadhi ya wafuasi wa CCM, Nyimbo na Nyagawa walijijengea mizizi iliwafanya wawe maarufu ndani na nje ya Chama katika maeneo yao.

Katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, Nyimbo ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Njombe Magharibi mwaka 1995 hadi 2005, alishika nafasi ya kwanza, lakini alienguliwa kugombea hivyo kuamua kujitoa na kujiunga na CHADEMA.

Nyagawa kwa upande wake, alikuwa mwiba mkali hata kwa aliyekuwa Mbunge wa siku nyingi wa Njombe na baadaye Njombe Kaskazini, Makwetta. Aliamua kujiengua CCM baada ya kudai kuwa kulikuwa na ukukwaji wa taratibu katika kura za maoni hivyo kutokuridhishwa na hali hiyo.

Jambo kubwa ambalo wana CCM wengi bado wanajiuliza ni kwa nini CCM ilishindwa katika jimbo la Iringa Mjini, licha ya kutangazwa kwamba wanachama waliokuwa wakigombea nafasi hiyo walivunja makundi yao na kuwa kitu kimoja.

Katika jimbo hilo, wakati wa kura za maoni kulikuwa na mchukano kati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela, na aliyekuwa akitetea nafasi yake, Monica Mbega, licha ya kwamba walikuwepo wengine waliojitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Mwakalebela ndiye aliyeibuka mshindi katika mchuano huo uliowahusisha wana CCM sita. Licha ya kuibuka mshindi, alienguliwa kuwa mgombea kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya madai ya kujihusisha na rushwa. Vikao mbalimbali kuanzia wilaya, mkoa  hadi taifa vilikata jina lake na kumteua Monica kugombea ubunge.

Hatua hiyo ya kuenguliwa Mwakalebela ilisababisha mgawanyiko mkubwa katika Chama, hatua ambayo iliwafanya vijana waliokuwa wafuasi wa mgombea huyo kumnadi Mchungaji Msigwa. Hata jitihada mbalimbali zilizofanyika za kuyaunganisha makundi hayo zilishindikana.

Rais Kikwete alipokwenda Iringa kwenye kampeni, kwa mfano, alimsimamisha Mwakalebela jukwaani katika Uwanja wa Samora na kusema amevunja kambi yake hivyo wafuasi wake wampigie kura Monica. Hiyo ilionekana kuwa CCM ni kitu kimoja kumbe ilikuwa sawa na kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa!

Uchunguzi uliofanywa unaeleza kuwa kitendo cha Rais kumsimamisha Mwakalebela kilichochea zaidi hasira za wapigakura hasa vijana. Inadaiwa kuwa wakati wa kinyang’anyiro cha kura za maoni, vijana waliitwa kila aina ya majina mabaya kama vile ‘wahuni’, ‘wavuta bangi’ na ‘vibaka’, jambo ambalo liliwakasirisha sana.

Hata wakati wa kuweka mikakati ya kuhakikisha CCM inashinda, makundi hayo yakiwemo ya madereva teksi na wafanyabiashara katika soko kuu la Iringa Mjini, yalikataa kukutana na Monica na viongozi wa Chama kwa kile kilichodaiwa kutukanwa.

“Sasa wametutambua kuwa sisi ni nani. Walituita wahuni sasa wameujua uhuni wetu kuwa una maana. Tumewanyima kura ili watambue kuwa tuna uwezo wa kumuweka mtu au kumweka madarakani. Sasa Monica Mbega ameipata,” walisema madereva teksi wa stendi kuu ya mabasi ya mikoani.

Licha ya kuenguliwa kwa mwakalebela kuwa ni chanzo cha vijana wengi kutokuipigia CCM, kuwepo kwa makundi yanayohasimiana kisiasa ni sababu kubwa.

Kwa muda mrefu Iringa imekuwa na kundi linalojiona ndilo linaloweza kuamua lolote na hatimaye likawa. Kundi hilo linajiita ‘Iringa Network’.

Kundi hilo linahusisha wanasiasa wakongwe, waliowahi kushika nafasi mbalimbali serikalini na kwenye mashirika muhimu ya umma pamoja na wafanyabiashara. Kundi hilo ndilo linalodhani kuwa lolote linaloamua ndilo litakuwa hata kama umma haukubaliani na matakwa yao.

Kutokana na vitendo hivyo, baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakigombea nafasi mbalimbali, walikuwa wakitakiwa wawaone kwanza ili wapate baraka zao. Kinyume cha hapo wataambulia patupu katika azma yao ya kugombea nafasi yoyote.

Wapo watu ambao ni wahanga wa kundi hilo kwa kukatwa majina yao kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM, ubunge na udiwani. Mtu anayetakiwa na kundi hilo, atafadhiliwa kwa gharama zozote, mradi tu ashinde. Viongozi wa Chama wanaokwenda kufanya kazi katika mkoa huo, huwekwa mikononi mwa kundi hilo hivyo kufanya c
chochote  wanachokitaka.

Katika uchaguzi wa CCM wa mwaka 2007, kwa mfano, kundi hilo lilifanya kila jitihada mtu wao ashinde katika nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia mkoa. Hata hivyo lilishindwa baada ya mgombea wao kushika nafasi ya tatu.

Kadhalika katika uchaguzi huo, walimtaka aliyekuwa mweka hazina wa mkoa kuendelea na nafasi hiyo licha ya tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili. Hatimaye mgombea wao alishindwa.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka huu, kundi hilo lilijipanga kuhakikisha watu wanaowaweka katika majimbo ya Kilolo, Kalenga, Iringa Mjini, Mufindi Kaskazini, Makete na Ludewa wanafanikiwa kupenya na hata wakishindwa wanapitishwa.

Jaribio hilo lilishindwa Kalenga baada ya aliyekuwa mgombea wao kushindwa na hata kudiriki kuchakachua matokeo. Walimtumia aliyekuwa katibu wa wilaya kufanya kazi hiyo kwa gharama yoyote lakini nguvu ya umma iliwashinda aliyeshinda kihalali kutangazwa mshindi.

Pia katika majimbo mengine walishindwa baada ya wagombea wao kutupwa vibaya na walioshinda kwenye majimbo hayo- Profesa Msolla (Kilolo), Mahamoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini) na Menrad Kigola.

Kwa pande wa Iringa Mjini walifanikiwa kwani walihakikisha Mwakalebela anaenguliwa na kila ngazi wanaweka mizizi yao ili kufanikisha azma waliyojiwekea. Na kweli walifanikiwa kwani hata hoja waliyoiwasilisha taifa, iliungwa mkono kwa madai kwamba mgombea huyo anatuhumiwa kujihusisha na vitndo vya rushwa.

Suala hilo walipoulizwa wananchi jimboni walisema madai hayo yalikuwa na lengo la kujikosha kwani aliyekuwa akitoa rushwa ya waziwazi ikiwemo kugawa kanga na vitenge ni mgombea waliyemtaka.

“Malipo yake wameyaona sasa. Mgombea waliyempandikiza ameshindwa na tuko tayari kukaa miaka mitano bila mbunge, waende wakajifunze kuwa utamlazimisha punda kwenda kisimam I lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji,” walisema kubainisha kwamba matakwa yao hayakuwa na mashiko kwa wananchi.

Hiyo ndiyo hali halisi iliyoifanya Iringa Mjini kwenda upinzani baada ya miaka 10 kuwa mikononi mwa CCM. Ubabe, chuki binafsi, matakwa ya kundi la watu wanaodhani kila watakalo litatimia, ndicho chanzo cha CCM kuboronga.

Mwisho   

    


                           

No comments:

Post a Comment