Tuesday, November 23, 2010

KWA HILI CCM IJISAHIHISHA

OKTOBA 31, mwaka huu, ulifanyika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ambapo Rais Jakaya Kikwete, alichaguliwa tena kuongoza nchi.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rais Kikwete alipata kura 5,276,827 sawa na aslimia 61.17 ya kura zote halali zilizopigwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania.

Wagombea wengine waliojitokeza kugombea nafasi hiyo ni Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Hashim Rungwe (NCCR Mageuzi), Peter Mziray (APPT Maendeleo), Fahmi Nassor Dovutwa (UPDP) na Mugahywa Muttamwega wa TLP).

Katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Slaa alipata kura 2,271,941 (asilimia 26.34), Profesa Lipumba kura 695 (asilimia 8.06), Fahmi Nassoro Dovutwa kura 13,176 (asilimia 0.15), Peter Mziray kura 96,933 (asilimia 1.12), Hashim Rungwe kura 26,388 (asilimia 0.31) na Mugahywa Muttamwega kura 17,482 sawa na asilimia 0.20.   

vile vile, katika uchaguzi wa Wabunge na Madiwani, CCM ilizoa viti vingi hivyo kupata nafasi ya kuunda serikali kwa maana ya serikali kuu na halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya. Hata hivyo, ziko sehemu chache ambazo vyama vya upinzani vilifurukuta hivyo kupata fursa ya kuunda halmashauri.

Pamoja na kupata ushindi huo wa kishindo, matokeo ya mwaka huu yameleta hisia tiofauti kwani CCM imepoteza viti vya ubunge na udiwani katika maeneo ambayo ilikuwa ikiyashikilia.

Hata katika kura za urais, Rais Kikwete alipata kura chache kulinganisha na alizopata mwaka 2005. katika uchaguzi wa mwaka 2005, Rais Kikwete alipata kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.2 ya kura halali zilizopigwa, akifuatiwa kwa mbali na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF ambaye alipata kura 1,327,125 (asilimia 11.7).

Kitarakimu, kura alizopata Rais Kikwete, zimepungua kwa kiasi cha kura 3,846,125 kulinganisha na zile za mwaka 2005, licha ya kwamba waliojitokeza mwaka huu walikuwa wachache tofauti na uchaguzi uliopita.

Kwa upande wa ubunge, baadhi ya maeneo ambayo imepoteza ni (Ilemela, Nyamagana na Ukerewe (Mwanza), Mbeya Mjini na Mbozi Magharibi (Mbeya) na Karatu na Arusha Mjini (Arusha).

Mengine ni Vunjo, Rombo na Hai (Kilimanjaro), Kilwa Kusini na Lindi Mjini (Lindi), Iringa Mjini (Iringa), Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Mjini na Kasulu Vijijini (Kigoma), Biharamulo (Kagera), Maswa Magharibi, Maswa Mashariki, Bukombe na Meatu (Shinyanga).

Pia CCM imepoteza Mbulu (Manyara), Biharamulo (Kagera), Singida Mashariki (Singida), Kawe na Ubungo (Dar es Salaam) na Musoma Mjini (Mara).

Vile vile kwa visiwani, imepoteza majimbo matatu ya Magogoni, Mwanakerekwe na Mtoni nap ia kushindwa kukomboa jimbo la Mji Mkongwe lililo katika himaya ya CUF.

 Pamoja na kupoteza majimbo hayo, CCM imefanikiwa kukomboa jimbo la Tarime lililokuwa chini ya CHADEMA miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo, CCM imeshindwa kuyakomboa majimbo ya Mpanda Mjini, Moshi Mjini ambayo yamekuwa yakishikiliwa na CHADEMA, Mji Mkongwe (CUF), Bariadi Mashariki (UDP) na mengine 18 ya Pemba.

CHANZO NINI?
Kupoteza majimbo mengi kwa kiasi hicho, kumesababisha mjadala miongoni mwa wachambuzi na hata baadhi ya watu kuanza kudhani kuwa mustakabali wa uhai wa CCM sasa uko shakani.

Zipo sababu nyingi zilizofanya kuwepo kwa hali hiyo ambazo CCM inapaswa kuzifanyia kazi ili kuhakikisha yaliyotokea hayajirudii katika uchaguzi ujao.

Sababu kubwa iliyofanya majimbo mengi kwenda upinzani, na pengine kubwa kuliko zote, ni ubinafsi miongoni mwa viongozi hasa watendaji katika ngazi za wilaya na mikoa.

Watendaji hao, yaani makatibu wa mikoa, wilaya pamoja na wale wa jumuia za Chama, walishiriki kukihujumu chama hasa kwa kupendelea baadhi ya wagombea. Mfano katika hilo ni Dar es Salaam na Iringa.

Mkoani Dar es Salaam wana CCM katika majimbo ya Kawe na Ubungo waliamua kuwapigia kura wagombea wa CHADEMA na kuwatosa wale wa CCM.

Sababu kubwa iliyotolewa na wanachama hao ni kwamba wagombea wa CCM, Hawa Ng’humbi (Ubungo) na Angela Kizigha (Kawe) hawakuwa chaguo bali la viongozi wa Chama. Chaguo lao, kwa mujibu wa wanachama hao, walikuwa Nape Nnauye na Kippi Warioba.

Licha ya ubunge, suala la viongozi kuchakachua matokeo lilijitokeza katika kura za maoni za udiwani ambapo katika baadhi ya kata jijini Dar es Salaam waliopendekezwa si wale walioshinda katika kinyang’anyiro hicho.

Hiyo ilijidhihirisha katika kata za Miburani, Chang’ombe na Wailesi (Temeke) na Msewe (Ubungo) ambapo wanachama waliandamana hadi ofisi za CCM Mkoa kulalamikia uchakachuaji wa matokeo.

Katika kata ya Miburani, kwa mfano, wanachama waliandamana kumkataa Fortunatus Mang’wela (aliyekuwa diwani kabla ya kura za maoni) kwa madai kuwa hakuwa chaguo lao bali waliyemchagua alikuwa Juma Mkenga.

Mkoani Iringa nako, kulikuwa na kizaazaa katika majimbo ya Iringa Mjini na Kalenga. Kalenga, kwa mfano, aliyekuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Iringa Vijijini, Luciano Mbossa alidaiwa kumpendelea wazi wazi Abbas Kandoro  wakati wa kura za maoni.

Ilidaiwa kuwa katibu huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji katika wilaya kwa maana ya viongozi wa Chama na jumuia, na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Wilaya, walifanya kila njia kuhakikisha Kandoro anashinda.

Hata matokeo yalipotoka na kuonyesha kuwa mgombea waliyembeba ameshindwa dhidi ya Dk. William Mgimwa, bila aibu, walianza kupita usiku kwenye baadhi ya kata na kubadilisha matokeo ili mtu wao aonekane ameshinda.

Azma yao hiyo ilifanikiwa na kumtangaza Kandoro kuwa mshindi. Lakini kutokana na Dk. Mgimwa kujua ndiye aliyeshinda, alisimama kidete na kuhakikisha haki inatendeka na hatimaye kutangazwa mshindi.

Jambo kama hilo pia lilijitokeza katika jimbo la Iiringa Mjini ambapo viongozi wa CCM wilaya kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa mkoa chini ya Katibu wa Mkoa, Mary Tesha,  walimwengua Frederick Mwakalebela aliyekuwa ameshinda na kumpendekeza Monica Mbega.                    
       
Viongozi hao walifanikiwa kuishawishi Kamati ya Siasa ya Mkoa na vikao vya Chama ngazi ya taifa kumwengua mshindi huyo wa kura za maoni. Madai waliyoyatoa ni kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Hali hiyo iliwashangaza wananchi wengi wa jimbo la Iringa na kuapa kuwa uonevu huo dhidi ya mgombea wao wataulipizia kwa njia ya kura. Ndivyo walivyofanya katika kura kama waklivyoahidi kwa  kumchagua Mchungaji Peter Msigwa wa CHADEMA. Kwa kufanya hivyo, CCM ikakosa mwana na maji ya moto.

UAMUZI WA WANANCHI
Kwa kawaida viongozi wanachaguliwa na wananchi, kama misingi ya demokrasia inavyobainisha. Kwa mantiki hiyo, uamuzi wa wananchi unapaswa kuheshimiwa na ndivyo CCM ilivyopaswa kufanya hivyo.

Hiyo pia ilielezwa bayana na viongozi wa ngazi za juu wa CCM wakiwemo Mwenyekiti Rais Kikwete na makamu wake, Pius Msekwa. Viongozi hao walisema Chama kitaheshimu uamuzi wa wananchi na kwamba watakaoshinda kwenye kura za maoni, ndio watakaopitishwa kugombea.  

Ni kweli katika maeneo mengi, CCM ilifanya hivyo. Lakini katika baadhi ya maeneo watu waliolalamikiwa kuwa ama walishinda kwa mizengwe au kubebwa na viongozi wa mikoa na wilaya, walipitishwa.

Hatua hiyo iliwafanya wanachama kuwapigia kura wagombea wa upinzani, ikiwa ni majibu kwa Chama kutokuheshimu matakwa yao.         

Mfano dhahiri ulioonyesha kuwa wananchi waliamua kuihukumu CCM ni katika jimbo la Bukombe, Shinyanga, ambapo Profesa Kulikoyela Kahigi, aliyejiengua CCM na kuhamia CHADEMA baada ya kura za maoni, aliibuka kidedea dhidi ya Emmanuel Luhahula ambaye alilalamikiwa kuwa hachaguliki lakini Chama kilimpitisha.

Hali hiyo pia ilitokea katika Maswa Magharibi ambapo baadhi ya viongozi wa mkoa na wilaya walimfanyia mizengwe John Shibuda, aliyekuwa mbunge. Shubuda alijiunga na CHADEMA na hatimaye wananchi kumpa ridhaa ya kurejea bungeni.

KUZINGATIA UTAFITI
Jambo lingine ambalo limesababisha CCM kupoteza majimbo mengi, ni kutokufanyia kazi taarifa mbalimbali zikiwemo za utafiti kama ile ya Mpango wa Utafiti wa Elimu na Demokrasia (REDET) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

REDET, katika utafiti wake, ilieleza kuwa wabunge 143 kati ya 232 waliokuwemo katika bunge lililopita kutoka majimbo ya uchaguzi hawachaguliki, hivyo kuwa vigumu kurejea bungeni baada ya uchaguzi mkuu.

Utafiti wa taasisi hiyo, iliyo chini ya Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, ulionyesha kuwa  asilimia 61.7 ya wabunge wasingechaguliwa tena. Kwa upande wa Rais pia, ilielezwa kuwa Rais Kikwete angeweza kupata asilimia 66.9.

Sababu kubwa iliyotolewa na wananchi waliohojiwa ni utendaji wa wabunge hao majimboni Kwa maana hiyo, wananchi walionyesha kuchoshwa na utendaji wao na kwamba wanaridhika nao kwa asilimia 38.

Matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 31, mwaka huu kwa kiasi fulani, yamelingana na utafiti wa REDET kwani Rais amepata asilimia 61.17 ambayo ni tofauti ya asilimia 5.73. Wabunge wa zamani ambao hawakurudi majimboni ni asilimia  57.7, ambayo ni tofauti ya asilimia nne kulinganisha na ile ya REDET.

Kutokana na taarifa za utafiti kama ile ya REDET, CCM ilipaswa kuifanyia kazi na kuhoji ni kwa nini inatokea hivyo, badala ya kuamini tu kuwa itaibuka na ushindi wa kishindo kama si wa mafuriko.  

MAKUNDI HATARI
Ndani ya CCM, kuna makundi ya wanachama na viongozi, jambo ambalo ni sababu ya kushindwa kwa Chama katika baadhi ya nafasi kwenye uchaguzi.

Mkoani Iringa, kwa mfano, kuna kundi linaloundwa na wanasiasa na wafanyabiashara walioko ndani na nje ya mkoa huo, maarufu kama ‘Iringa Network’. Kundi hilo, kwa mtazamo wake, linadhani bila wao hakuna kinachoweza kufanyika na kwamba wao ndio Iringa na Iringa ni wao.

Mtu anapotaka kugombea ubunge, mathalan, anatakiwa awaone ndipo apate baraka zao. Vile vile, kundi hilo huhakikisha kila mtendaji (makatibu wa mkoa na wilaya) anayepelekwa huko, anawekwa mikononi mwao na kutekeleza matakwa yao.   

Watu hao ndio waliochangia kwa kiasi kikubwa CCM kupoteza jimbo la Iringa Mjini. Ndio waliohakikisha kwa gharama zozote Mwakalebela anaenguliwa. Walifanikiwa lakini nguvu ya wananchi iliwapa fundisho kwa mgombea wao kupigwa chini.

Makundi kama ‘Iringa Network’ yapo kila sehemu na hayo ni sumu kubwa kwa ustawi na maendeleo ya Chama katika ngazi zote. Kuendelea kwa makundi kama hayo kunaweza kukimaliza Chama.   

Licha ya makundi, ili kubadilika, CCM haina budi kwenda hali halisi ya sasa. Ni lazima itambue kuwa kizazi cha sasa ni tofauti na cha miaka 10 au 15 iliyopita, na hiyo ni changamoto kubwa.

Uelewa katika kizazi cha sasa uko juu kulinganisha na miaka 10 hadi 15. Kuna ongezeko kubwa na wasomi kutokana na kuibuka kwa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, hivyo uwezo wa kupembua na kuchanganua mambo umeongezeka. Kwa mantiki hiyo, CCM lazima ihame kutoka mtandao wa ‘analogue’ na kwenda kwenye ‘digital’.

Ni dhahiri kwamba kama CCM itatekeleza na kujisahihisha katika mambo haya na mengine, Watanzania watajenga imani zaidi na kuendelea kuichagua. Kinyume cha hapo mambo yatakuwa tofauti.   

No comments:

Post a Comment