Wednesday, November 10, 2010

KATE KAMBA, MAKINDA, ANNA ABDALLAH WAPITISHWA USPIKA

WANASIASA wanawake wakongwe watatu wa CCM, Anne Makinda, Kate Kamba na Anna Abdallah, wamepitishwa na Kamati Kuu ya CCM Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yussuf Makamba aliwaambia waandishi wa habari hivi punde mjini Dodoma kuwa wanasiasa hao wanawake ambao wamekuwa katika nyadhifa mbalimbali tangu serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere hadi sasa, wamependekezwa na Kamati Kuu kuwania nafasi hiyo.

Kinamama hao sasa watapigiwa kura na Wabunge wa Kamati ya CCM hapo kesho ili kupata jina moja ambalo litawasilishwa katika Bunge kwa ajili ya kupigiwa kura sambamba na wagombea wengine kutoka vyama vya siasa ili kumpata kinara wa chombo hicho ambacho ni moja ya mihimili mitatu ya dola.

Makamba katika taarifa yake hiyo alisema Kamati Kuu imeamua kuwapendekeza wanawake ili kuheshimu maazimio mbalimbali ya kimataifa juu ya usawa wa kijinsia.

"Kamati Kuu imeamua kuwapendekeza wanawake hao kugombea nafasi hiyo kwani tangu uhuru, mihimili yote mitatu imekuwa ikiongozwa na wanaume. Kamati Kuu imependekeza mwanamke ili kuongoza mhimili huu ambapo itakuwa mara ya kwanza Bunge kuongozwa na Spika mwanamke.

"Kamati Kuu imeamua kwamba wakati umefika kuwa mhimili huu wa tatu kwa maana ya Bunge uongozwe na mwanamke," alisema.

Habari zaidi zinasema mshindi kati ya kinamama hao atashindana na wagombea wa upinzani akiwemo Mabere Marando, aliyependekezwa na CHADEMA kuwania nafasi hiyo.

Nafasi ya Spika wa Bunge kwa miaka mitano iliyopita ilikuwa ikishikiliwa na Samuel John Sitta aliyepata umaarufu wa kuliongoza Bunge kwa VIWANGO NA KASI.

Wasifu kuhusu wagombea wa nafasi ya Uspika kupitia CCM utapatikana muda si mrefu kupitia 'blog' hii.

   

No comments:

Post a Comment