NA MAURA MWINGIRA, NEW YORK
WATANZANIA wana mksemo mbalimbali ambayo hutumika kufikisha ujumbe fulani. Moja ya misemo hiyo ni ‘mzigo mzito mpe Mnyamwezi’.
Msemo huo unasadifu na jukumu alilopewa aliyekuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dk. Augustine Mahiga, la kuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Somalia .
Ni heshima kubwa si kwa Balozi Mahiga kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo, lakini pia ni heshima kwa Tanzania na Watanzania wote. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon katika angaza angaza yake, hakumwona mtu mwingine wa kumkabidhi mzigo mzito, zaidi ya Balozi Mahiga.
Tayari Dk. Mahiga ameianza kazi hiyo ya kusimamia na kuhakikisha Somalia inakuwa na amani baada ya kuwa katika hali tete kwa takriban miaka 20 sasa.
Baada ya kukabidhiwa jukumu lile, Balozi Mahiga alifungasha virago vyake na kuhamia Nairobi , Kenya ambako ndiko ziliko ofisi zake.
Mwanzoni mwa Septemba, mwaka huu, Dk. Mahiga alifika mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutoa taarifa yake ya kazi ya kile ambacho amekiona, amekifanya na nini anashauri kifanyike. Katika taarifa yake, Balozi Mahiga alianza kwa kutoa tahadhari kubwa kuhusu mwelekeo wa nchi ya Somalia .
Alisema: “Kadri Umoja wa Mataifa unavyoendelea kusuasua kuongeza kasi ya kuisaidia serikali ya mpito ya Somalia, kuvisaidia vikosi ya kulinda amani vya Umoja wa Afrika (AMISOM), kiintelejensia, kijeshi kwa maana ya vifaa vya kisasa na askari wa kutosha wa kulinda amani, ndivyo Somalia inavyozidi kutumbukia katika kuwa kitovu cha ugaidi wa kimataifa”,
Katika kauli yake hiyo, hakuzungusha wala hakutaka kuremba maneno na kusema dalili za Somalia kuwa kitovu cha ugaidi zimekwishaanza kujitokeza na ziko wazi.
“Uzoefu unaonyesha kwamba kadiri tunavyoendelea kuchelewa au kutoa ushirikiano mdogo kuhusu tatizo la Somalia , ndivyo hali inavyozindi kuwa ngumu na ya kutisha nchini humo. Lazima tuamue sasa kuzikabili kwa dhati changamoto zinazoikabili Somalia ,” alisema.
Alitahadharisha kuwa kuwepo kwa vitendo vya ugaidi wa kimataifa katika kanda ya Afrika ya Mashariki, kumejidhihirisha kwa matukio ya milipuko ya mabomu Kampala , Uganda Julai, mwaka huu na shambulio la bomu liliofanyika katika hoteli ya Muna , Somalia, wakati wa mwezi wa Ramadhani..
Kutokana na hali hiyo, alisema Umoja wa Mataifa kupitia Baraza lake la usalama, hauna budi kuingilia kati kwa kukamata silaha na wapiganaji wanaoingia nchini Somalia kupitia bandari ya Kismayu ambayo kwa sasa inashikiliwa na kundi la Al Shaabab
Ndani ya muda huo, kumekuwa na serikali za mpito 19, ambazo zimekuwa zikianguka au kuangushwa moja baada ya nyingine. Ni Somalia hii ambayo dunia ilishuhudia matukio ya kutisha waliyofanywa na wanajeshi wa Marekani walioingia kujaribu kuweka sawa hali ya mambo.
Kwa sasa, Somalia si Somalia tena. Raia wake wametawanyika pembe zote za dunia, na huku mamia kwa maelefu wakiwa wakimbizi wa ndani ya nchi yao . Inajulikana katika jumuia ya kimataifa kama nchi iliyoshindikana.
Lakini mbaya zaidi na ambalo linaitisha jumuia ya kimataifa, ni balaa la sasa ambalo nchi hiyo inaelekea kuwa kitovu cha ugaidi. Hali hii inaziweka mahali pagumu nchi za Afrika Mashariki na za Pembe ya Afrika.
Kupanuka kwa ugaidi wa kimataifa, uharamia na hali mbaya ya kibinadamu nchi Somalia , kunahitaji nguvu kubwa za ushirikiano kutoka jumuia ya kimataifa. Pia inahitajika mkakati madhubuti wa kuzuia wimbi la uingizwaji wa silaha nchini humo.
Bandari ya Kismayu, kwa mujibu wa Dk. Mahiga, si tu inapitisha silaha haramu, bali pia inatumika kuingiza dawa za kulevya na wapiganaji wa kujitoa mhanga wanaotoka mataifa mengine.
Kwa sasa, Somalia iko chini ya utawala wa serikali ya mpito inayoongozwa na Sheikh Sharif Sheikh Ahmed lakini kumekuwapo na taarifa mbalimbali zinazoonyesha kuwa serikali hiyo ya mpito si tu kwamba haina nguvu au ubavu wa kupambana na makundi yanayopingana nayo likiwamo kundi la Al Shabaa, bali pia kumekuwapo na mvutano na sintofahamu miongoni wa viongozi ndani ya serikali.
Udhaifu huo umefanya serikali hiyo inayosaidiwa na uwepo wa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika kutawala sehemu ndogo tu ya nchi hiyo. Kama hiyo haitoshi, kundi la Al Shabaab ambalo inasadikiwa kuwa na uwezo mkubwa kijeshi, limeendelea kuchukua maeneo mengi .
Baada ya jumuia ya kimataifa kushindwa kupeleka wanajeshi wa kulinda amani Somalia , viongozi wa Umoja wa Afrika waliamua kwa kauli moja kulibeba jukumu hilo . Uganda na Burundi zilikuwa nchi za mwanzo kutoa vikosi vyake.
Pamoja na nia hiyo njema, na kufanya kazi katika mazingira magumu, vikosi hivyo vinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za ukosefu wa zana za kisasa na askari kutolipwa mishahara kwa wakati na kwa kiwango cha kuridhisha.
Hali hiyo imewafanya viongozi wa Afrika kupitia umoja wao, kuiomba jumuia ya kimataifa hususani Umoja wa Mataifa kuviongezea nguvu vikosi hiyo.
Msimamo mkubwa wa viongozi hao ni kwamba jukumu la kuilinda Somalia , ni la Umoja wa Mataifa na si Afrika pekee. Viongozi hao wanaweka bayana kwamba Afrika iko yatari kutoa askari wa kutosha kwenda kupelea lakini ni lazima Umoja wa Mataifa utimize wajibu wake wa kusaidia kwa hali na mali .
Kauli hiyo ya viongozi wa Afrika, imepewa nguvu au kuongezewa uzito na Balozi Mahiga hasa aliposema: “Uwezo wa kijeshi wa vikosi hivi unahitaji kuimarishwa kwa kusaidiwa na jumuia ya kimataifa. Malipo kwa askari lazima yalingane na ya wenzao walio katika operesheni zingine. Vikosi hivi vinahitaji vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kutekeleza majukumu yao hasa maeneo ya vijijini ambako mazingira yake ni magumu.”
Suala la kuitaka jumuia ya kimataifa kuongeza kasi ya kuvisaidia kwa hali na mali vikosi vya Umoja wa Afrika linapigiwa chapuo sana na viongozi wa ngazi zote na hususan wale wanaotoka Afrika.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya kwa nyakati tofauti wamekuwa wakilipigia debe kwa nguvu zote umuhimu wa vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia kusaidiwa.
Kwa mfano, aliyekuwa Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, amekuwa akisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halina budi kusaidia jukumu hilo huku akisisitiza kuwa mazingira magumu na ya hatari yanayowakabili wanajeshi wa Burundi na Uganda walioko Somalia, unaziogopesha nchi zingine kupeleka wanajeshi wake.
“Kuna nchi sita zimejitolea kutoa wanajeshi ili kuongeza nguvu. Lakini wanaona Waganda na Warundi wanavyoteseka, na hali hii inawatisha. Ni vyema basi jumuia ya kimataifa ikatekeleza mapema ahadi yake ya kutoka vifaa na fedha ili nchi nyingi zaidi zijitolee kupeleka watu wake,” alisisitiza Membe.
Alifafanua kuwa ingawa Afrika kupitia AMISOM imekwenda Somalia kwa ajili ya kulinda amani, jukumu hilo si la Afrika peke yake bali ni la jumuia ya kimataifa, kwa maana ya Umoja wa Mataifa.
Naye aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Moses Wentangula, hakuwa nyuma katika kutilia mkazo jambo hilo pale aliposema: “Kama si majeshi ya Umoja wa Afrika kutoa ulinzi kwa serikali ya mpito ya Somalia, hapana shaka kwamba Al Shaaba wangekuwa wameshaishika Somalia yote.”
Hata hivyo, alisema tatizo la Somalia si uwepo au wingi wa wanajeshi wa kulinda amani bali ni kukosekana kwa utashi kutoka jumuia ya kimataifa, huku akionya kwamba ikitokea serikali ya mpito ya Somalia ikaangushwa na Al Shabaab kushika nchi, basi sehemu kubwa ya eneo la Afrika Mashariki na pembe ya Afrika itakuwa katika hatari.
Wetangula alisema ni matumaini yake kwamba kutokana na hali tete ilivyo ndani ya Somalia na tishio la ugadi wa kimataifa unaoibukia, hapana shaka jumuia ya kimataifa sasa itaamka na kuwajibika ipasavyo.
Hali tete na tishio la ugaidi wa kimataifa unaoibukia Somalia , si tu kwamba unawatia hofu viongozi wa Afrika hasa wale wa Afrika Mashariki na pembe ya Afrika, lakini kwa kuwa ugaidi huo umevaa sura ya kimataifa, unawatia hofu hata wakubwa wengine duniani.
Wakichangia taarifa ya Dk. Mahiga, wajumbe wa Baraza la Usalama si tu waliunga mkono hoja ya kutaka vikosi vya Afrika na serikali ya mpito wasaidiwe, bali walionyesha wasiwasi juu ya kuibuka wa ugaidi wa kimataifa ndani ya Somalia .
Kutokana na hali hiyo, walitaka na kutoa wito kwamba wakati umefika wa Umoja wa Mataifa kutoa ushirikiano wa dhati kabla hali ya mambo haijafikia hali ya kushindikana kabisa.
Hapana shaka kuwa Umoja wa Afrika umetimiza wajibu wake, na umekuwa tayari kuongeza vigosi ya kulinda amani hadi kufikia 2,000. Lakini kama anavyosema Membe, moyo huo wa kujitolea wa Umoja wa Afrika utakwama kama jumuia ya kimataifa haitawajibika.

