Monday, February 28, 2011

MAKATIBU WAKUU WA WIZARA HAOOO

Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu watano wapya na kuwahamisha wengine wanne kutoka wizara moja kwenda nyingine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana  na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, uteuzi na uhamisho huo unaanza mara moja.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba mabadiliko hayo yametokana na muundo mpya wa Serikali ambako Wizara ya Miundombinu imegawanywa katika wizara mbili, na baadhi ya Makatibu Wakuu kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete amemteua  Fanuel E. Mbonde kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi Mbonde alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wengine walioteuliwa ni Hussein  Kattanga - Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; John M. Haule - Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Herbert Mrango - Wizara ya Ujenzi na  Eric K. Shitindi - Wizara ya Kazi na Ajira.

Kabla ya uteuzi wake  Kattanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Haule alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,  Mrango alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi , Shittindi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kwa upande wa waliobadilishwa vituo vyao, Rais Kikwete amemhamisha  Sazi  Salula kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenda Ofisi ya Makamu wa Rais, Maimuna  Tarishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii.

Pia  Injinia Omar  Chambo anahamia Wizara ya Uchukuzi akitokea Wizara ya zamani ya Miundombinu na Kijakazi  Mtengwa -anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Taarifa ilieleza kwamba  kuwa Dk. Ladislaus  Komba, aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anapangiwa kazi maalum katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Aidha,  Rais Kikwete amemhamishia  Elizabeth  Nyambibo Wizara ya Fedha na Uchumi ambako anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliyoachwa wazi na  Haule. Kabla ya uhamisho  Nyambibo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo  Makatibu Wakuu wanatarajia kuapishwa  leo saa tatu  Machi
00000


Sunday, February 20, 2011

WATANZANIA TUACHANE NA FIKRA ZA KUAJIRIWA, TUWAZE KUJIAJIRI

NA EPSON LUHWAGO
WAHITIMU wa kada mbalimbali nchini, wametakiwa kuondokana na dhana ya kuajiriwa pindi wanapomaliza masomo yao na badala yake wafikirie kujiajiri.
Rai hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye, wakati wa mahafali ya pili ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ghomme, iliyoko Ununio nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Simbeye alisema Watanzania wengi wanapomaliza masomo yao, hufikiria kuajiriwa, jambo ambalo linasababisha miongoni mwao kukosa ajira kwa vile nafasi za kazi ni chache.
“Watanzania wanafikiria kujiajiri baada ya kustaafu, sasa tujitahidi kubadilisha mawazo haya ili twende na wakati wa sasa,” alisema.
Alisema Watanzania waanze kubadilika na kufikiria kujiajiri badala ya kuajiriwa kwa sababu hivi sasa fursa ziko nyingi zinazotoa mwanya wa kujitegemea.
Naye Mkurugenzi wa Shule, Dk. Emmanuel Malangalila, alisema licha ya kuwa na muda mfupi tangu kuanzishwa, shule hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kitaaluma.
Alisema katika matokeo ya kidato cha sita mwaka jana, wanafunzi wanne waliohitimu walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Kwa upande wa kidato cha nne mwaka jana, Dk. Malangalila alisema wanafunzi wote 20 waliofanya mtihani walifaulu na wanatarajiwa kujchaguliwa kuingia kudato cha tano.
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 12 walihitimu kidato cha sita na Mkurugenzi huyo alisema kutokana na rekodi za kitaaluma, ana matumaini kuwa wote watafaulu na kuendelea na masomo ya elimu ya juu

GEORGE MLAWA ACHARUKA

NA EPSON LUHWAGO
KATIBU wa zamani wa Bunge, George Mlawa, ameshauri serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, kufanya uchunguzi wa kina kuhusu wanafunzi wengi kufeli mtihani wa kidato cha nne.
Akizungumza wakati wa mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ghomme, Dar es Salaam, juzi, Mlawa alisema serikali inatakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa sababu matokeo hayo kwa mwaka jana, hayana ishara nzuri.
“Kama zaidi ya asilimia 88 ya wanafunzi wamepata daraja la nne na sofuri, hapo yapo matatizo makubwa na si suala la kunyamazia au kutoa majibu rahisi hata kidogo,” alisema.
Kwa mtazamo wake, alisema tatizo linalofanya wanafunzi wengi kufeli ni kushindwa kumudu Kiingereza ambayo ni lugha ya kufundishia kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Alisema wanafunzi wengi wanaoingia kidato cha kwanza wanaanza kujifunza masomo kwa Kiingereza katika hatua hiyo, jambo ambalo anafikiri inakuwa vigumu kuimudu.
Kutokana na hali hiyo, alisema wanafunzi wanakuwa hawako tayari kukabiliana na masomo hivyo ni vyema serikali na wadau wakakaa na kujadili kama kuna uwezekano wa kuamua kufundisha masomo yote kwa Kiswahili kasoro somo la Kiingereza.
“Ukienda China, Russia na Ujerumani wanafunzi wanalazimishwa kutumia lugha za mataifa hayo. Kwa nini nasi tusitumie Kiswahili kama wenzetu? Hiyo ni changamoto kwangu kwa serikali na wadau wa elimu,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa shule za mchepuo wa Kiingereza zinaweza kuamua kutumia lugha hiyo kwa kuwa zimeshawajenga wanafunzi wao na wengi wanaijua vyema.
Mbali na lugha, Mlawa alisema tatizo lingine ni Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) kuwataka wanafunzi wanaorudia mitihani kufanya mitihani tofauti na wanafunzi wengine.
Licha ya kubadilisha mtihani, alisema NECTA pia imekuwa ikiwakomoa wanaorudia kutokana na kuongeza alama ya ufaulu kutoka 41 hadi 51.
“NECTA iondoe kikwazo hiki kwani hii haina maslahi yoyote kwa maendeleo ya nchi hii. Kama haitaondoa tutegemee wanafunzi kufeli zaidi.
Mwisho