Sunday, October 31, 2010

MSOLLA AKIPIGA KURA

Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Kilolo, Iringa, Profesa Peter Msolla, akipiga kura katika kituo cha Mazombe Shuleni. (Picha na Epson Luhwago)
Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Kilolo, Iringa, Profesa Peter Msolla, akipiga kura katika kituo cha Mazombe Shuleni. (Picha na Epson Luhwago)

MSOLLA AKIPIGA KURA

MGOMBEA Ubunge wa CCM katika jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla, akipiga kura katika kituo cha Mazombe Shuleni. (Picha na Epson Luhwago  

UCHAGUZI IRINGA WAFANYIKA KWA AMANI

Na Epson Luhwago, Iringa
KAZI  ya kupiga kura katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani mkoani Iringa, jana ilifanyika kwa amani na utulivu huku watu wengi wakiwa wamejitokeza kwa wingi.
Katika jimbo la Iringa Mjini, tangu asubuhi kulikuwa na misururu mirefu ya watu ambao walikuwa wakisubiri kupiga kura. Licha ya vituo kufunguliwa saa moja, wananchi walianza kumiminika vituoni tangu saa 12.30 asubuhi.
Katika maeneo ya Kitanzini, Frelimo, Gangilonga na Mshindo, mwandishi wa habari hii alikuta misururu ya watu waliokuwa wakisubiri kupiga kura.
Hata katika jimbo la Kilolo maeneo ya Mazombe, Mbigili, Lundamatwe na Ilula, kulikuwa na watu wengi katika vituo vya kupigia kura huku askari wa polisi na wale wa mgambo wakiwa wamejizatiti kwa ulinzi.
Baadhi ya wagombea, wakiwemo wa ubunge, walipiga kura kwenye vituo walivyojiandikisha. Mgombea ubunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla, alipiga kura saa 5.10 katika kituo cha Mazombe Shuleni, akiwa ameongozana na mke wake, Violet.
Katika upigaji kura wa jana katika maeneo mbalimbali ambayo mwandishi wa habari hii alipita, hakukuwa na fujo wala malalamiko kutoka kwa wapigakura. Walielezea kufurahishwa na usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ngazi za majimbo.
Wananchi ambao majina yao yalikuwa hayajabandikwa kwenye matangazo, walisema walifika vituoni na kuwaeleza wasaidizi ambao waliwasaidia na kupiga kura kwa kuwa majina yao yalikuwa kwenye madaftari ya kudumu ya wapigakura.
Naye Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Iringa, Barnabas Ndunguru, alisema kazi ya upigaji kura ilifanyika kwa amani na utulivu mkoani kote.
Wananchi 785,192 kutoka majimbo 11 ya mkoa wa Iringa, walitarajiwa kupiga kura kwa ajili ya Rais, Wabunge na Madiwani.
Wakati uchaguzi huo ukiwa umefanyika, tayari wagombea wanne wa ubunge wa CCM wamepita bila kupingwa. Wagombea hao ni Mahamoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini), Menrad Kigola (Mufindi Kusini), Anne Makinda (Njombe Kaskazini) na William Lukuvi (Ismani).
             

Tuesday, October 26, 2010

NIPENI HUYU NIFANYE NAYE KAZI

Mgombea ubunge jimbo la Kilolo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Peter Msolla akimnadi mgombea udiwani wa kata ya Ihimbo, Hezron Nganyagwa katika mkutano wake wa mwisho kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Mgombea ubunge jimbo la Kilolo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Peter Msolla akiwa na baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM mara badaa  ya kuvishwa mgolole na wazee wa kimila wa kata ya Ihimbo, ikiwa ni ishara ya kumtawaza kuwa kiongozi wao katika bunge lijalo.

MSOLLA KATIKA VAZI LA KICHIFU



Mgombea ubunge jimbo la Kilolo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Peter Msolla akivishwa mgolole na wazee wa kimila wa kata ya Ihimbo, ikiwa ni ishara ya kumtawaza kuwa kiongozi wao katika bunge lijalo.


Saturday, October 23, 2010

MAMBO YA TASAF NACHINGWEA

WANAFUNZI  wa Shule ya Msingi Muungano mkoani Lindi, wana kila sababu ya kufurahia mazingira ya kujisomea baada ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga madarasa mapya.

Madarasa hayo, yatakuwa chachu ya wanafunzi wa shule hiyo kupenda masomo tofauti na yale ya zamani ambayo yalikuwa yamechakaa kiasi cha kukatisha tamaa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga, alisema hivi karibuni kuwa majengo hayo ni sehemu ndogo ya kazi iliyofanywa na Mfuko wake kwa miaka kadhaa iliyopita, lengo likiwa ni kutekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii.

Mwamanga, alisema ujenzi wa madarasa hayo umefanyika kupitia udadhili wa OPEC.

TASAF ni mshirika mkubwa wa maendeleo ya jamii katika kuwaletea Watanzania maisha bora kwenye sekta mbalimbali kama vile uwezeshaji wananchi kiuchumi hasa kwa jamii zilizo masikini, afya kwa maana ya ujenzi na ukarabati wa zahanati na elimu.    


Madarasa haya ni sehemu ya mchango wa TASAF katika kuboresha elimu nchini. Haya ni madarasa yaliyoko katika Shule ya Msingi Muungano huko Lindi

TASAF yaboresha elimu Nachingwea

MAENDELEO ya elimu mara nyingi hutokana na sababu mbalimbali zikiwemo walimu wa kutosha, vifaa kama vile madawati na vitabu pamoja na madarasa ya kutosha.

Ndiyo maana katika maeneo mengi nchini hasa vijijini, kumekuwa na matatizo hayo ambayo huchangia kiwango cha elimu kuporomoka.

Vile vile mazingira ya sehemu ambapo shule ipo kwa maana ya majengo huchangia wanafunzi na hata walimu kuwa na ari ya kupenda masomo na kazi.

Majengo ya shule ambayo ni chakavu au yaliyojengwa kwa miti na kuezekwa nyasi, hayawezi kuwa kichocheo kwa wanafunzi kufanya vizuri. Au shule ambayo wanafunzi wake wanasomea chini ya mti hawawezi kuwa na ari ya kusoma kwa sababu mazingira hayawafanyi wapende kusoma.

Hali hiyo ni tofauti na inavyokuwa katika shule zenye majengo mazuri, yenye madawati ya kutosha na zenye walimu wanaoishi katika nyumba nzuri na vitabu vya kiada na ziada vya kutosha.

Katika shule kama hiyo, mwalimu kwa vyovyote vile atakuwa na ari ya kufanya kazi. Hata wanafunzi pia watakuwa na ari ya kusoma kwa bidii. Matokeo yake, kiwango cha ufaulu kitakuwa juu, hivyo kuchangia kukua kwa sekta ya elimu nchini.

Mikoa ya kusini hususan Lindi na Mtwara, imekuwa na matatizo mbalimbali katika sekta ya elimu yakiwemo ya uhaba na uchakavu wa majengo, ukosefu wa walimu kutokana na mazingira yaliyokuwepo (kabla ya kuimarika kwa miundombinu) na mila potofu zilizokuwa zikifanyika huko.

Kutokana na matatizo hayo, wanafunzi wengi walikuwa wakiishia ama kutoroka, kuolewa au kukimbilia mijini kufanya biashara ndogo ndogo maarufu kama ‘umachinga’.

HIVI NDIVYO hali ilivyokuwa katika Shule ya Msingi Muungano huko Nachingwea Mkoani Lindi. Madarasa haya yalikuwa hayatoi fursa ya wanafunzi kupenda masomo.

Hatua hiyo iliifanya serikali kuhimiza maendeleo ya elimu kupitia mipango mbalimbali kama ule wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na wa sekondari (MMES).

Chini ya mipango hiyo, shule zimejengwa katika maeneo ambayo hayakuwa nazo hivyo kuwezesha watoto waliokuwa wakikosa nafasi za kusoma kuzipata. Pia shule za sekondari katika maeneo mbalimbali zimejengwa hivyo kuwezesha wale wanaopata nafasi ya kujiunga na elimu hiyo kupata nafasi.

katika  shule za msingi, majengo mengi yalikuwa yamechakaa kiasi cha kukatisha tamaa hata walimu kufundisha. Hatua hiyo ilisababisha wanafunzi kufeli.

Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa na tatizo kama hilo kwa muda mrefu. Lakini kupitia mpango wa serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, hali imeanza kuwa nzuri.

MKONO WA TASAF
Moja ya shule ambazo zilikuwa katika hali mbaya kwenye wilaya hiyo ni Muungano. Majengo yake yalikuwa chakavu kiasi cha kuwafanya walimu na wanafunzi kukosa hamu ya kufundisha na kusoma.

Lakini serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imefanya kile kinachotakiwa na kurejesha ari kubwa katika shule hiyo.

Selemani Lidume, mwalimu katika shule hiyo alikuwa shahidi katika kuonyesha kuwa mazingira mazuri ni chanzo cha elimu bora, baada ya TASAF kujenga vyumba vipya vya madarasa shuleni hapo.

Muungano ni moja ya shule ambazo zimenufaika na miradi ya TASAF ambayo jamii yenyewe imekuwa ikiiibua na mfuko huko kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji.

Mwalimu Lidume alisema majengo hayo mapya yatakuwa kichocheo cha kuongeza kiwango cha elimu katika shule hiyo. Alisema kiwango cha ufaulu kinatarajiwa kuongezeka kwa kuwa wanafunzi watakuwa na ari ya kusoma zaidi kwa sababu mazingira yameboreshwa.



“Tazama, hapa sijivuni wala sijigambo, lakini ukweli ni kwamba majengo haya mapya yenye vyumba vine vya madarasa ni kichocheo cha kuongeza kiwango cha ufaulu mwakani. Wanafunzi wana hamu ya kutumia madarasa haya ambayo yana madawati pia,” alisema.

“Jambo hili ambalo lilisubiriwa kwa hamu kubwa, litawafanya wanafunzi kujifunza kwa bidii zote. Ni ukweli usiofichika kwamba  sasa tunatarajia kuongeza kiwango cha ufaulu angalau kwa asilimia 80,” alisisitiza Lidume, mwalimu kijana na mtanashati alipoulizwa kuelezea alivyopokea jambo hilo.

Kujiamini huko kwa Lidume si kwa kutia chumvi katika kauli yake. Mwaka jana, kwa mfano, shule hiyo ilifaulisha wanafunzi 16 kati ya 32 waliomaliza darasa la saba na kujiunga katika elimu ya sekondari.

Kwa mantiki hiyo, kuwepo kwa madarasa mapya, kutatoa motisha zaidi kwa wanafunzi kusoma hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na shule za sekondari hapo mwakani. Hali hiyo pia, itawezesha hata walimu kuwa na ari ya kufundisha zaidi kwa sababu mazingira yameboreshwa.

“Kila mwalimu hujisikia vyema pale anapofundisha katika darasa ambalo lina kila kitu. Unatarajia nini kama unafundisha wanafunzi ambao wanakaa chini, au wanafunzi wane au watano wamebanana kwenye dawati moja? Kwa sasa nasema wzi kwamba tumeukata kuwa katika hali hii,” alisisitiza.

Upanuzi wa shule hiyo ambao ulifanywa ndani ya miezi sita, ulikamilika Septemba, mwaka huu. Kwa sasa kazi iliyobaki ni kukamilisha kuweka samani kama vile madawati 60 na meza za walimu.

Kazi hiyo hadi ambayo imefanywa kwa msaada wa TASAF kupitia mfuko wa OPEC, hadi kukamilika kwake, itagharimu sh. 32,142,980. TASAF na OPEC wametoa sh. 25,695,340 na wananchi wamechangia sh. 6,447,640.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea,  Mariam Mtunguja, alipongeza kazi hiyo na kuwa itaongeza kasi ya maendeleo ya elimu wilayani humo.

Alisema mchango unaotolewa na TASAF kupitia OPEC katika sekta za elimu, barabara, mifugo na afya ni mingi na imesaidia kupunguza matatizo yanayoikabili jamii nchini.

Licha ya elimu, TASAF wilayani Nachingwea imesaidia katika miradi mbalimbali 32 ambayo kwa ujumla wake, imegharimu zaidi y sh. milioni 647.

PROFESA MSOLLA KATIKA MICHEZO

PROFESA MSOLLA akitoa zawadi kwa nahodha wa timu iliyoshinda katika Bonanza la Michezo la Krismasi lililofanyika mwaka 2009 katika kijiji cha Lukani, wilayani Kilolo. Michezo hiyo ilidhaminiwa na Mwanakilolo kutoka katika kijiji hicho, Danford Mbilinyi.

KAMANDA WA VIJANA KILOLO

MBUNGE  wa Kilolo, Profesa Peter Msolla (wa pili kulia) akiwa amevaa rasmi joho la ukamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Kilolo baada ya kutawazwa rasmi. aliyenyoosha mikono ni Venance Mwamoto aliyekuwa Kamanda kabla ya Msolla na kulia kwake ni Sethi Moto, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilolo ambaye ni kaka wa damu wa Mwamoto. Kulia ni Deo Sanga a.ka. Jah People, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, ambaye alimtawaza Profesa Msolla kuwa Kamanda.

PROFESA MSOLLA KAZINI

PROFESA Msolla akishiriki katima moja ya shughuli za maendeleo katika jimbo la Kilolo

MSOLLA NA ASKOFU MDEGELLA

PROFESA Msolla akisalimiana na Askofu Dk. Owdenburg Mdegella wa KKKT Dayosisi ya Iringa katika moja ya shughuli za kidini ambazo Profesa Msolla alikuwa mgeni Rasmi.Ukaribu wa viongozi hao umewezesha kupatikana maendeleo kwa kasi ndani ya Kilolo na Iringa kwa jumla

HUYU NDIYE PROFESA MSOLLA

PROFESA PETER MSOLLA, Mbunge wa Kilolo na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia akiwa amevalia mavazi rasmi ya kichifu ya kabila la Wahehe. Hiyo ni kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya katika kipindi chake cha ubunge miaka mitano iliyopita.

PROFESA MSOLLA ACHANJA MBUGA KILOLO

KUNA kila dalili kuwa mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Kilolo mkoani Iringa, Profesa Peter Msolla,  atashinda kwa kishindo katika kinyang’anyiro hicho.

Zipo sababu nyingi zinazofanya kuwe na uhakika. Kwanza wapinzani wake ni dhaifu kwa maana kwamba hawana nguvu kama alizo nazo Profesa Msolla na pili, uwezo wao wa kujenga hoja wawapo jukuwaani.

Wagombea wanaochuana na Profesa Msolla ambaye ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ni Claudy Mwitula wa CHADEMA na Mwaka Mgimwa wa CHAUSTA.

Lakini kubwa zaidi, Profesa Msolla amemaliza karibu maeneo yote ya jimbo hilo kwa kufanya kampeni wakati wapinzani wamekwenda sehemu chache tu kutokana na uwezo wake kirasilimali.

Huyu ndiye Profesa Msolla, msomi na mwanazuoni aliyeifanya Kilolo kuwa juu kimaendeleo
Kubwa kuliko yote hayo, Profesa Msolla katika miaka mitano iliyopita akiwa Mbunge ameweza kusimamia mambo mengi ambayo yameonekana dhahiri na ni ya maendeleo.

Katika tarafa ya Kilolo, moja ya tarafa tatu katika jimbo hilo, idadi kubwa ya wananchi walikuwa katika umasikini wa kutisha kutokana na kuishi katika maisha duni.

Lakini kumekuwa na mabadiliko ndani ya miaka mitano aliyokaa katika nafasi ya ubunge. Na hiyo ndiyo sababu iliyowafanya wana CCM ndani ya jimbo hilo kumpa kura za kishindo wakati wa kura za maoni dhidi ya wapinzani wake Venance Mwamoto na Stephen Mwaduma, ambao walikuwa Wabunge kuanzia mwaka 1988 hadi 2005.

Wananchi wa tarafa hiyo katika baadhi ya maeneo, walikuwa hawana usafiri wa uhakika kwani walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 20 au zaidi kutoka kwenye makazi yao hadi kwenye kituo cha basi Kidabaga ili waweze kupanda basi kwenda Iringa mjini na sehemu zingine. Lakini sasa inawezekana kwani basi sasa linafika hadi Idete.

Ndani ya kipindi hicho pia Profesa Msolla ambaye nimsomi gwiji katika tiba ya mifugo na mwanataaluma wa muda mrefu, ameweza kuwaunganisha wana Kilolo wa maeneo mbalimbali na kuwa kitu kimoja.

Sifa nyingine kubwa ambayo ameipata ni kuhakikisha Kilolo inakoma kuwa kiwanda cha kuzalisha wasichana wa ndani (house girls) wanaofanya kazi katika miji mbalimbali.

Hiyo inatokana na juhudi zilizofanyika za kujenga shule za sekondari katika kata. Kwa sasa Kilolo ina shule za sekondari 39 zikiwemo zile zinazomilikiwa na mashirika ya dini hasa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa.    

     

MBEYA, RUKWA NI KIKWETE TU URAIS

NA MWANDISHI WETU
UTAKELEZAJI  wa miradi ya maendeleo uliofanywa na serikali ya CCM katika miaka mitano iliyopita, ndio tiketi ya Rais Jakaya Kiketwe kupata kura za kishindo Oktoba 31, mwaka huu. 

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Kampeni za CCM katika Mkoa wa Mbeya, Dk. Chrisant Mzindakaya, alipokuwa akiwahutubia wananchi katika mikutano mbalimbali ya kampeni mkoani humo hivi karibuni.

Katika mikutano hiyo, Dk. Mzindakaya alisema ushindi wa kishindo wa Rais Kikwete katika uchaguzi huo utatokana na namna alivyotekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za mwaka 2005 na zile zilizoko katika Ilani ya Uchaguzi ya miaka mitano iliyopita.

“Kwa maana hiyo, Rais Kikwete hatoi ahadi zisizotekelezeka, anatafsiri Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 ambayo Ilani inaelezea utekelezaji wa dira hiyo. Kwa hiyo mtu anaposema nchi imekosa mwelekeo, anakuwa hatendi haki kwa kuwa serikali ya CCM imetekeleza yote hayo,” alisema.

Mzindakaya alisema ahadi nyingi alizotoa Rais Kikwete katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini- Iringa, Mbeya, Rukwa na Katavi, zimetekelezwa kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana wananchi wa mikoa hiyo watampa kura za kishindo na kupata nafasi ya kuongoza nchi kwa miaka mingine mitano ijayo.

Miongoni mwa ahadi alizotekeleza kwa zaidi ya asilimia 90 katika mikoa hiyo, kwa mujibu wa Dk. Mzindakaya, zimo katika sekta za elimu, afya na miundombinu.

Kwa upande wa elimu kwa mfano, mkoani Mbeya, alisema mwaka 2005 alipoingia madarakani, kulikuwa na wanafunzi 20, 371 waliojiunga na kidato cha kwanza lakini mwaka huu wameongezeka hadi kufikia wanafunzi 138, 747, idadi ambayo ni zaidi ya mara tano.

Katika miundombinu, alisema mkoani Mbeya barabara ya Mbeya- Chunya- Makongolosi ambayo itafika hadi Tabora, inajengwa kwa kiwango cha lami, sambamba na ile ya kutoka Mpemba hadi Ileje. Barabara nyingine ni ya kutoka Kyela- Ipinda hadi Matema Beach, katika Ziwa Nyasa.               

Mkoani Rukwa, Dk. Mzindakaya alisema barabara zinazounganisha mkoa huo (pamoja na mpya wa Katavi, ulioanzishwa kwa kumegwa sehemu ya Rukwa na Tabora) na mingine zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Alizitaja barabara hizo kuwa ni Tunduma- Sumbawanga; Sumbawanga- Mpanda; na Sumbawanga- Kasanga kupitia Matai ambazo tayari makandarasi wako kazini.

MAMIA ya wananchi wakiwa katika mkutano wa kampeni wa Kikwete. Wananchi kama hawa Mbeya na Rukwa wamesema wao ni Kikwete tu kwa urais

Kukamilika kwa barabara hizo kwa kiwango cha lami, kutaifanya mikoa ya Rukwa na Katavi kupiga hatua kubwa kimaendeleo miaka michache ijayo. Pia kero ya usafiri katika mikoa hiyo, alisema itakuwa historia.

Vile vile, alisema bandari ya Kasanga inapanuliwa ili iweze kutoa huduma kwa kiwango cha juu katika kushughulikia mizigo inayotoka Tanzania na nchi jirani Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda na Burundi.

“Sasa ukiangalia yote haya, utajua wazi kuwa ni maendeleo makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Kikwete ndani ya miaka mitano. Na hii ndiyo tiketi ya kumpa tena ridhaa ya kuongoza tena nchi,” alisema.

Dk. Mzindakaya pia alisema mafanikio mengine yamepatikana katika Azimio la Iringa la mwaka 1972 la Siasa ni Kilimo ambalo linaitwa Kilimo Kwanza, lenye lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo na kuwawezesha Watanzania kuondokana na umasikini.

Alisema chini ya mpango huo, wananchi wameanza kupatiwa pembejeo za ruzuku kwa njia ya vocha na matokeo yake yameanza kuonekana.

Kupitia mpango huo, alisema mavuno ya mazao ya chakula yameanza kuongezeka. Katika mkoa wa Mbeya, kwa mfano, alisema mavuno yamepanda kutoka tani milioni 3.3 kwa mwaka huu kulinganisha na tani milioni 2.4 ya msimu uliopita.

Kwa upande wa Rukwa, alisema mwaka huu mavuno yalikuwa tani milioni mbili wakati mwaka jana yalikuwa tani milioni 1.6. mwaka 2005 tani milioni 1.2 zilivunwa.

Mafanikio hayo ambayo yanalenga la kutimiza melengo ya milenia katika kutokomeza njaa na utapiamlo, yataelendelea kuwepo kutokana na mipango ya serikali ya utoaji wa pembejeo za ruzuku. Alisema mkoani Rukwa mavuno katika msimu ujao yanatarajiwa kuongezeka baada ya serikali kutoa ruzuku ya sh. bilioni  nane.

Alisema jambo lingine ambalo linampa sifa Rais Kikwete ya kuchaguliwa tena, ni ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha dawa za kuua mazalia ya mbu mjini Kibaha, Pwani.

Sambamba na kugawa chandarua, alisema ujenzi wa kiwanda hicho utakaopanza mwishoni mwa mwaka ujao, ambao utagharimu dola za Marekani milioni 23 (karibu sh. bilioni 30) utawezesha Tanzania kutokuwa na mbu kabisa hivyo kuifanya huru dhidi ya malaria.

“Hizi ndizo ahadi za kweli zinazotolewa na Rais Kikwete kupitia Ilani ya CCM na kwa maana hiyo, ni dhahiri atapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Oktoba 31, mwaka huu,” alisisitiza.

Mzindakaya pia alisisitiza kuwa mwaka 2005, Rais Kikwete alikuwa na sifa tatu ambazo ni mgombea wa CCM, mnadi Ilani ya Chama na mtu anayeuzika. Lakini sasa, alisema sifa zake zimeongezeka zikiwemo za uadilifu katika kuongoza nchi, kutekeleza vizuri Ilani na kuifanya Tanzania kujulikana na kuheshimika katika jumuia ya kimataifa.

“Kwa sifa hizo, Kikwete anastahili kuchaguliwa tena. Watanzania katika hili lazima wajue kwamba hatuchagui watu kwa majaribio kwenda Ikulu bali kwa kuangalia uzoefu ambao Kikwete anao.

“Kabla ya kuwa Rais, Kikwete alikuwa Waziri kwa miaka 17 hivyo ndiye pekee anayestahili kwani wagombea wengine hawajawahi kushika hata unaibu waziri, hivyo hawana sifa za nafasi ya urais,” alisema.

Mwisho       
                   

Monday, October 18, 2010

MZINDAKAYA ALIPOWAAGA WAPIGAKURA WAKE

MZINDAKAYA akiwahutubia wananchi wa Kwela katika kijiji cha Msanda Muungano.
HII ni sehemu ya umati uliofika Msanda Muungano kumuaga Dk. Mzindakaya baada ya kustaafu siasa. Mkutano huu ulihudhuriwa na mamia ya watu.

WANAKWELA WALIPOMUAGA MZINDAKAYA


MAPEMA mwaka huu, mwanasiasa mkongwe nchini, Dk. Chrisant Mzindakaya, alitangaza kuwa anaachana na siasa baada ya kuwa katika medani hiyo kwa miaka 45.
Mzindakaya akiwa na mbunge mwenzake na kiongozi ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama na Serikali, Paul Kimiti, walisema umefika wakati wa kung’atuka katika siasa ili kupisha wengine wafanya makubwa zaidi. Walitoa taarifa hiyo Sumbawanga, mkoani Rukwa mbele ya waandishi wa habari na wanachama na viongozi wa CCM.
Hatimaye walihitimisha azma yao hiyo ya kung’atuka walipoaga rasmi mjini Dodoma wakati wa bunge la Bajeti, Juni hadi Julai, mwaka huu, ambalo lilikuwa likihitimisha uhai wake wa miaka mitano kuanzia mwaka 2005.
Wanasiasa hao waliaga kwa staili ya aina yake kwa kutoka katika jengo la Bunge mjini Dodoma huku wakipunga mikono kuonyesha ishara ya ‘Kwaheri’.
Hata hivyo, Mzindakaya (70), aliona si busara kutokuwaaga wapigakura wake wa jimbo la Kwela, ambao walimfanya awe mbunge wao kwa miaka 15 tangu mwaka 1995.
Kabla ya hapo, aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Sumbawanga (wakati huo likiwa jimbo moja tu katika wilaya za Nkasi na Sumbawanga) na pia kuwa mbunge kutokana na nafasi yake ya ukuu wa mkoa.  
Dk. Mzindakaya aliwaaga rasmi wana Kwela Agosti 21, mwaka huu kijijini kwao Msanda Muungano. Sherehe hizo zilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Kwa hakika, siku hiyo ilikuwa ya kipekee kwa mwanasiasa huyo ambaye ameweka alama ya kukumbukwa ndani ya bunge, serikali, Chama na kwa wananchi wa Rukwa na Tanzania kwa jumla.  
Msafara wa kutoka Sumbawanga mjini kwenda Msanda Muungano, ulianza saa 4.30 asubuhi na kuwasili katika eneo la Kibaoni, njia panda ya kwenda kijijini huko, umbali wa kilomita tano, saa 5.25.
Mzindakaya katika msafara huo aliongozana na mkewe Teddy, baadhi ya watoto wake, wadogo zake na ndugu, jamaa na marafiki wa karibu.   
Baada ya kufika hapo ilibidi msafara huo usimame  kumsubiri Mkuu wa Mkoa ambaye alikuwa nyuma ili aweze kuongozana na Dk. Mzindakaya na ujumbe wake.
Hatimaye Njoolay aliwasili saa sita mchana na msafara kuanza rasmi huku ukiongozwa na pikipiki 20 zilizokuwa zikiendeshwa na vijana waliovaa sare za CCM.
MAPOKEZI MAKUBWA
Baada ya kuwasili Msanda Muungano, msafara huo ulipokewa na wananchi waliokuwa wamefurika kwenye uwanja wa mikutano wakitumbuizwa na vikundi vya kwaya na ngoma.
“Twakupokea baba Mzindakaya, twakupongeza kwa kazi nzuri uliyoifanya. Kustaafu kwako ni heshima kubwa na inapendeza kwa kazi nzuri uliyofanya kwa jimbo la Kwela.” Hayo ni baadhi ya maneno yaliyokuwa katika nyimbo zilizoimbwa wakati wa hafla hiyo baada ya kuwasili kijijini hapo.
Wanakwaya hao waliendelea kuelezea yaliyofanyika katika jimbo la Kwela, ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari Unyiha, iliyoko kijijini hapo na kituo cha afya cha Msanda pamoja na kuhimiza uboreshaji wa sekta ya kilimo.
Walisema mambo kama hayo aliyafanya alipokuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mbeya, Kigoma na Rukwa. Katika kilimo, walisema aliwafundisha kupanda mahindi kwa mstari tofauti na walivyokuwa wakifanya wao kwa kutupa mbegu tu shambani.
“Mwaka 2010 umeamua kupumzika mwenyewe, pole na kazi. Watuacha na majonzi la kufanya tumekosa, Mungu akulinde,” ndivyo walivyomaliza wanakwaya hao.
Mengi yaliyofanywa na mwanasiasa huyo yalisemwa zaidi katika risala iliyosomwa na wanakijiji cha Sandulula yakiwemo maendeleo katika sekta za afya, maji, elimu na kilimo.
Ili kumkumbuka zaidi, wananchi wa Sandulula na Msanda Muungano waliamua kumzawadia ng’ombe wanne, mbuzi wane, gunia la mahindi na zawadi za kimila.
HATIMAYE ALONGA
Baada ya hapo Dk. Mzindakaya alisimama na kuzungumza na wananchi wa Kwela waliokuwa wamefika katika hafla hiyo ya kumuaga, ambayo binafsi alisema si ya kuaga bali ni ya kurejea rasmi nyumbani baada ya utumishi wake wa miaka 45.
“Nimeamua kustaafu siasa na kurejea nyumbani mkiwa bado mnanipenda na hakuna mtu ambaye angenishinda kama ningetaka kuendelea Kuwa mbunge wenu, lakini nimeamua niache mwenyewe kwa heshima,” alisema.
Kutokana na uamuzi wake huo, aliwaasa wanasiasa nchini kujenga utamaduni wa kung’atuka wakiwa bado wanapendwa na wananchi ili waendelee kuheshimiwa. Alisema uamuzi wake wa kung’atuka umetokana na nia ya kujenga heshima aliyojiwekea.
“Ni vyema watu wajue kwamba baada ya muda fulani ni lazima waondoke katika nafasi zao. Kwa kufanya hivyo, watajenga heshima, badala ya kung’ang’ania na mwisho wake kufedheheka,” alisisitiza.
Alisema baada ya kukaa katika ubunge na nafasi mbalimbali za uongozi kwa miaka muda wote huo, ameona ni vyema akae pembeni na kuwapisha wengine ili waendeleze pale alipoishia.
“Miaka 45 katika utumishi ni mingi na nimefanya mengi. Kwa nini ning’ang’anie? Naondoka huku nafurahi,”  alisema.
Pamoja na kustaafu, alisema amejivunia mambo mengi aliyoyafanya katika taifa, ikiwa ni pamoja na kuendeleza kilimo katika mikoa aliyoiongoza alipokuwa mkuu wa mkoa hususan Morogoro, Mbeya, Kigoma na Rukwa.
Alisema mambo hayo yamemfanya aendelee kukumbukwa na wananchi wa mikoa hiyo na taifa kwa jumla.
Kwa upande wa Rukwa, alisema yapo mambo ya kihistoria ambayo atakumbukwa nayo. Moja ya mambo hayo, kwa mujibu wa Mzindakaya, ni elimu.
Dk. Mzindakaya alisema enzi zake wilaya ya Sumbawanga (kabla ya kugawanywa na kupatikana Nkasi na sasa wilaya mpya ya Kalambo), ilikuwa na shule ya sekondari ya Kantalamba pekee lakini sasa zipo 140. Alisema hayo ni maendeleo makubwa ambayo Sumbawanga imepiga katika elimu.
Vile vile alisema maendeleo ya kilimo katika mkoa wa Rukwa yamechangiwa na nafasi yake kwa kuwa aliwahimiza kulima kwa kutumia njia za kisasa pamoja na maksai badala ya jembe la mkono.
Alisema wakati huo wananchi walikuwa wanalima kwa njia za kizamani lakini aliamua kuwaelekeza namna ya upandaji kwa mstari na utunzaji ili kupata mavuno bora.
“Kwenye afya ndiyo usiseme. Zahanati hazikuwepo na shangazi yangu amefariki dunia bila kuona dawa ya hospitalini, lakini sasa kila sehemu kuna zahanati na vituo vya afya,” alitanabahisha.
NJOOLAY AMFAGILIA 
Njoolay alimmwagia sifa kemkem kwa kusema Dk. Mzindakaya anastaafu siasa na uongozi akiwa ameweka kumbukumbu ya kudumu miongoni mwa Watanzania.
Alisema sifa ambazo mwanasiasa huyo mkongwe atakumbukwa nazo ni ujasiri wa kujenga hoja na kuzitetea, kujali maslahi ya taifa na kupenda maendeleo.
“Mzindakaya akisimamia jambo ambalo ana uhakika nalo... huwezi kumtoa katika mstari. Watanzania watamkumbuka alipokuwa hodari wa kuibua maovu ya viongozi na wakawajibika. Ana uwezo wa kuzungumza jambo kwa uhakika kwa kuwa ana takwimu na takwimu zake si za ubabaishaji,” alisema.
Kati ya mwaka 1995 na 2005, ndani ya Bunge, aliwahi kuibua hoja kadhaa nzito ambazo ziliwafanya baadhi ya waliokuwa mawaziri kujiuzulu. Mawaziri hao ni Iddi Simba (Viwanda na Biashara) na Profesa Simon Mbilinyi (Fedha) pamoja na Naibu wake, Kilontsi Mporogomy.
Waziri mwingine aliyeponea chupuchupu ni Shamsa Mwangunga (Maliasili na Utalii) kwa  kukiuka azimio la Bunge juu ya leseni za uwindaji katika vitalu.
Njoolay alisema Mzindakaya ni mpenda watu, mpenda maendeleo na wakati wote akili yake huzungumzia masuala ya maendeleo tu na si vinginevyo.
“Leo tunazungumzia mapinduzi ya kilimo lakini yeye alianza tangu zamani kule Morogoro alipokuwa RC (mkuu wa mkoa). Kigoma aliwafurahisha na sasa wananufaika na michikichi kwani zile ni juhudi zake alipokwenda Malaysia,” alisema Njoolay.
Uwezo wake katika kujenga hoja na kupenda maendeleo, alisema vimemfanya ajulikane kimataifa ndiyo maana vyuo vikuu vya Marekani vimentunuku shahada mbili za heshima za udaktari. Shahada hizo alitunukiwa mwaka 2004 na mwaka huu.
KUMBUKUMBU YA KUDUMU
DK. Mzindakaya katika maisha yake amekuwa akisisitiza umuhimu wa watu kuthubutu. Ameonyesha hilo kwa vitendo alipoamua kuanzisha kiwanda kikubwa cha nyama kilichopo Kizwite, manispaa ya Sumbawanga. Kiwanda hicho kwa mujibu wa wataalamu, ni kikubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Wakati mmoja aliwahi kusema Watanzania wengi hawana uwezo wa kuthubutu ndiyo maana maendeleo miongoni mwao ni ndoto. Lakini kama wangethubutu, alisema Tanzania ingepiga hatua kimaendeleo.
“Watu wanaogopa kuthubutu kwa sababu wanajua wakishindwa watalaumiwa na ndiyo maana wasiothubutu hawana cha kulaumiwa. Lakini tuliothubutu tupo na tumeonyesha umma na tumefanikiwa,” alisisitiza.
Akizungumzia maisha yake baada ya kustaafu siasa, Mzindakaya alisema atajihusisha na kilimo na ufugaji pamoja na kusumamia uendeshaji wa kiwanda chake ambacho anatarajia kuongeza shughuli ikiwemo utengenezaji wa vyakula vya wanyama.
vijana wenye pikipiki wakiusindikiza msafara wa Dk. Mzindakaya kwenda Msanda Muungano kwa ajili ya kuagwa. Hiyo ilikuwa Agosti 21, 2010.
   

HAKUNA LISILOWEZEKANA


FATMA Maghimbi akikaribishwa rasmi CCM na Rais Jakaya Kikwete kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita

Kama wahenga walivyosema hakuna adui wala rafiki wa kudumu katika siasa, ndivyo ilivyotokea Jumapili iliyopita baada ya wakongwe wawili wa siasa za vyama vingi visiwani Zanzibar Fatma Maghimbi na Juma Othman Juma baada ya kurudisha kadi zao za CUF na kuchukua za CCM. 

Wanasiasa hao walifanya hivyo jimboni Kawe jijini Dar es salaam wakati wa mkutano mkubwa wa hadhara uliohutubiwa na mgombea urais wa CCM, Mheshimiwa Dk. Jakaya Kikwete. 

Baada ya kupokea kadi zao mpya, Maghimbi na mwenzake walisema kama ni mvua basi hayo ni manyunyu, mvua kamili inakuja kwa maana kwamba wapo wenzao kibao  watafuata nyayo zao kutoka CUF.

Akielezea sababu zake za kurudi CCM, Juma Othman Juma amesema ameguswa kwa kazi kubwa aliyofanya Mheshimiwa Kikwete Tanzania Bara na Visiwani hususan aliporejesha amani na utulivu visiwani Unguja na Pemba kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alisema tangu historia ya vyama vingi ianze Tanzania, kila wakati wa uchaguzi wananchi wengi wa visiwa vya Unguja na Pemba hulazimika kukimbia visiwani humo kwa kuhofia hali ya kutokuwa na usalama katika kipindi hicho.

"Lakini sasa napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Kikwete kwa kurudisha heshima ya nchi yetu duniani kwani mwaka huu wa kampeni, hakuna hata mmoja aliyehama visiwani humo kukimbia uchaguzi" alimaliza Juma Othman akishangiliwa na umati mkubwa wa wana CCM waliojitokeza kwenye mkutano huo wa kampeni.

Mama Fatma Maghimbi amewahi kuwa waziri kivuli wa Katiba na Sheria ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa kama mbunge wa Chama Cha Wananchi CUF.

Naye Juma Othman Juma amewahi kuwa mwanzilishi wa Chama Cha Siasa visiwani kabla ya kujiunga na Chama cha Wananchi CUF.

Sunday, October 17, 2010

PROFESA MUSHI AMESEMA KWELI

MWANAZUONI gwiji wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samuel Mushi, amehoji yalipo meno ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Gwiji huyo ambaye baadhi ya wanazuoni ambao sasa ni maprofesa katika chuo kikuu hicho na vinginevyo ndani na nje ya Tanzania, alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa meno ya taasisi hiyo yamekuwa butu mapema baada ya kuonekana makali wakati wa mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea wa udiwani na ubunge hivi karibuni.

Alisema meno ya TAKUKURU yamekuwa butu mapema na kwamba ilikuwa nguvu ya soda tu.

Inawezakana maneno ya Profesa huyo ambaye ni mchambuzi wa masuala mbalimbali hasa katika fani ya siasa na utawala, yakawa kweli kutokana na ukweli kwamba yale yaliyotarajiwa na wananchi hayakutokea. Hiyo inatokana na taasisi hiyo kutangaza kwa mbwembwe kuwa imewakamata wagombea kadhaa wakati wa kura za maoni wakiwa na mabulungutu ya pesa na kwamba itawachukulia hatua za kisheria.

Habari juu ya kukamatwa kwa watu hao wakiwemo vigogo ambao miongoni mwao waliokuwa mawaziri katika serikali ikiwemo ya Rais Jakaya Kikwete zilivuma na kutikisa anga la Tanzania na watu kuamini kuwa sasa kumekucha.

Matukio hayo ya rushwa yaliripotiwa katima mikoa mbalimbali kama vile Rukwa, Arusha, Kilimanjaro, Iringa, Mwanza, Dar es Salaam na Tanga. Makamanda wa Taasisi hiyo kwenye mikoa hiyo walikuwa akizitangaza kwa mbwembwe lukuki kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na vidhibiti hivyo ingekuwa kazi rahisi kuwafikisha mahakamani na hivyo kukosa sifa za kuwa wagombea.

Cha ajabu ni kwamba kati ya waliokamatwa ni Joseph Mungai tu ambaye ametinga kizimbani kwa maana hiyo ndiye pekee amekuwa 'mbuzi wa kafara' al maarufu kama 'bangusilo' kama inavyojulikana kwa watu wa Pwani hususan Wazaramo.

Mbona wengine hawajafikishwa mahakamani na wanaendelea kupeta katika kampeni wakiomba kura kwa wananchi? Hapo ndipo hoja inapoanzia.

Kutokana na kuwepo kwa utata huo, ndipo inapoonekana kwamba hii si taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa bali ni TAASISI YA KUKUZA NA KUSTAWISHA RUSHWA kama Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakala la Richmond chini ya Dk. Harrison George Mwakyembe ilivyobainisha kutokana na ilivyojaribu kuficha ukweli juu ya kuwepo kwa mazingira ya mlungula  katika sakata hilo.

        

HII NDIYO HALI HALISI TUNDUMA-SUMBAWANGA WAKATI WA MASIKA

Abiria wa mabasi wakiwa wamekwama Machi, mwaka huu katika eneo la Tunduma kutokana na gari la mizigo kuziba njia, lilipojaribu kugeuka.
Magari ya abiria na mizigo yakiwa yamesongamana katika eneo la Isanga, Mbozi mkoani Mbeya, barabara ya Tunduma - Sumbawanga kutokana na kuharibika kwa barabara kwenye kijiji hicho kwea sababu ya mvua zilizokuwa zikinyesha Machi.  
Abiria wa mabasi ya kutoka Sumbawanga na Mbeya wakijaribu kusaidia kulikwamua lori la mafuta ili kuwezesha magari kupita katika kijiji cha Isanga.
Magari yakiwa yamekwama katika kijiji cha Isanga, Mbozi mkoani Mbeya kwenye barabara ya Tunduma- Sumbawanga kutokana na ubovu wa barabara. Abiria walikaa zaidi ya saa moja katika eneo hilo.
Gari la mafuta likiwa limekwama katika kijiji cha Isanga, barabara ya Tunduma- Sumbawanga wilayani Mbozi, Mbeya, kutokana na ubovu wa barabara uliosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha. Abiria wanaosafiri katika njia hiyo wamekuwa wakikwama katika maeneo mbalimbali ya barabara hiyo kwa sababu ya ubovu wa barabara uliosababishwa na mvua hivyo kufanya wasafiri kwa saa 12 au zaidi badala ya saa tano kati ya Tunduma na Sumbawanga. Wakati mwingine hulazimika kulala njiani.

HII NDIYO ADHA YA USAFIRI TUNDUMA-SUMBAWANGA WAKATI WA MASIKA

Magari yakiwa yamesongamana katika eneo la Tunduma baada ya gari la mizigo kuziba barabara na kusababuisha usafiri kati ya Tunduma na Sumbawanga kukwama kwa zaidi ya saa moja. Hiyo ilikuwa Machi mwaka huu. Nilikuwa mmoja wa waliopata misukosuko kipindi hicho

NEEMA YAJA KWA WANANCHI WA SUMBAWANGA

Ile adha ya muda mrefu kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa juu ya usafiri, sasa itatoweka baada ya kuwepo kwa habari njema kwamba makandarasi wa kujenga kipande cha barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga kupatikana.

Nakumbuka niliwahi kusota kipindi cha masika mwaka huu ambapo nilitoka Mbeya saa moja asubuhi na kufika sumbawanga saa mbili usiku. Barabara wakati huo ilikuwa mbaya kupindukia. Ushahidi juu ya hali ilivyokuwa angalia picha zinazofuata.

Lakini baada ya kilio cha muda mrefu, hatimaye serikali imeliona hilo na kuamua kulitekeleza kwa barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami na ili kuharakisha kazi hiyo na kukamilisha kwa haraka barabara hiyo yenye urefu wa takriban kilomita 244, imegawanywa kwa vipande vidogo vidogo.

Katibu Tawala wa mkoa wa Mbeya, Beatha Swai, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita katika kikao cha wadau kukabidhi barabara ya Tunduma-Sumbawanga kwa makandarasi wa ujenzi wa barabara ya Tunduma-Mkutano-Sumbawanga.

Kipande cha barabara kutoka Tunduma-Ikana, chenye urefu wa kilometa 63.7, kitajengwa na kampuni ya M/S Consolidated Contractors Group ya nchini Ugiriki kwa gharama ya shilingi bilioni 82.5.

Barabara nyingine ni kipande cha Ikana-Laela, chenye urefu wa kilometa 64.2, ambacho mjenzi wake ni M/S  China New Era International Engineering Corp.ya China, kwa gharama ya shilingi bilioni 76.1.

Ujenzi wa barabara hiyo ya Tunduma mkoani Mbeya hadi Sumbawanga, mkoani Rukwa umefadhiriwa na Millenium Challenge Coorparation ya Marekani kupitia kitengo chake cha Millenium Challenge Account (MCA-T).

“Mikoa ya Mbeya na Rukwa, kama ilivyo kwa mikoa mingine nchini huwa inakumbwa na tatizo la usafiri hasa katika kipindi cha mvua.Safari kati ya Tunduma na Sumbawanga huchukua saa nyingi na muda mwingine barabara hujifunga kabisa” alisema Beatha.

Aliongeza kuwa ni matumaini ya serikali, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 224, kwa kiwango cha lami itasukuma na kusaidia mabadiliko ya kiuchumi kwa mikoa hii miwili na nchi jirani.

Beatha alisema kuwa wananchi wa Mbeya na Rukwa, hawataweza kusahau siku ambazo walikuwa wanashindwa kuitumia barabara hiyo, hasa kipindi cha mvua, na hivyo ni imani kuwa barabara hiyo itachochea sera ya Kilimo Kwanza kukamilishwa.

Saturday, October 16, 2010

ZANA ZA ISIMILA

Hizi ni zana za zilizotumiwa na mwanadamu wa kale zilizoko Isimila, mkoani Iringa. (Picha hii imechukuliwa kutoka kwenye mtandao wa Internet, lengo likiwa ni kuwaonyesha watu baadhi ya zana hizo ambazo zinapatikana katika maonyesho hayo).
Hili ni bango linaloonyesha njia ya kwenda makumbusho ya zana za kale ya Isimila.

KABURI LA KIYEYEU

Hili ndilo kaburi la MZEE MARTIN KIYEYEU aliyefariki mwaka 1974, lililoko kando ya barabara ya Iringa-Mbeya katika kijiji cha Tanangozi, Iringa Vijijini mkoani Iringa. Ni kaburi ambalo liko mbioni kufanywa kuwa kivutio cha utalii.

KABURI LA KIYEYEU KUWA KIVUTIO CHA UTALII

Kwa wale watu wanaoishi au kutoka mkoani Iringa na wanaopita barabara ya Iringa- Mbeya eneo la Tanangozi, watakuwa wanalifahamu vyema kaburi la MARTIN KIYEYEU ambalo lina historia ndefu na ya ajabu.

Kaburi hilo limekuwa likielezewa kwa namna tofauti lakini ukweli ni kwamba inaelezwa kuwa kuna miujiza ya aina yake ambayo ilisababisha hata nyaya za umeme wa gridi ya taifa kushindwa kupita juu yake.

Ili kuweka kumbukumbu sahihi, mipango inafanywa ili kuhakikisha linakuwa moja ya vivutio vya utalii hapa nchini. Mikakati inayofanywa sasa ni kuhakikisha kaburi hilo, lenye historia na mazagazaga kibao, linatangazwa ndani na nje ya nchi ili liwe kivutio cha utalii.

Mmoja wa watu ambao wamekuwa wakizungumzia suala hilo ni Mgombea Ubunge wa CCM katika jimbo la Kalenga, Dk. William Mgimwa ambaye alisema kinachotakiwa ni kuweka mipango itakayowezesha kaburi hilo kuingia katika orodha ya vivutio vya utalii.

Mbali na kaburi hilo, maeneo mengine ambayo anaeleza kuwa ni ya muhimu katika kutangazwa ili yawe vivutio vya utalii ni jiwe la Igangidung'u (jiwe jekundu) lililoko Igangidung'u, makumbusho ya Mkwawa na Isimila ambako kuna zana za kale.

   

WANAKALENGA DAR WAMFAGILIA DK.MGIMWA

WANANCHI  wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa waishio Dar es Salaam, wamemfagilia mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Dk. William Mgimwa, kuwa ni mtu safi na atakayeleta maendeleo ya kweli na kuwawezesha wananchi kuondokana na umasikini unaowakabili.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema Dk. Mgimwa ameonekana ni mtu makini na mwenye kiu ya kuwaletea wananchi wa Kalenga maendeleo.

Mmoja wa watu walioelezea hayo ni Felix Mavika ambaye alisema CCM kumsimamisha mgombea huyo mtaalamu bingwa na msomi katika masuala ya benki na fedha, imefanya jambo la maana na kuwarejeshea wana Kalenga tumaini jipya la maendeleo.

"Dk. Mgimwa ni mtu mwenye uchungu na maendeleo ya jimbo la Kalenga, hivyo kitendo cha wana CCM katika jimbo la Kalenga kumpa kura nyingi wakati wa kura za maoni na Chama kumpitisha kuwa mgombea ni ushindi kwa jimbo la Kalenga," alisema.

Aliongeza kuwa kupitishwa kwake kutawawezesha kushirikiana katika kuchangia nguvu zao kwa ajili ya jimbo hilo lenye rasilimali nyingi lakini wananchi wake bado ni masikini.

Naye Mathew Kisinda alisema Dk. Mgimwa ni mtu mwenye upeo wa juu wa maendeleo hivyo kwa kuunganisha nguvu za wana Kalenga, ni dhahiri kuwa maendeleo yatapatikana.

"Kwa muda mrefu tulikuwa tunatafuta mtu ambaye ataunganisha nguvu za wananchi katika kuleta maendeleo ya jimbo letu. Kiu yetu imetimia na sasa tuna imani kuwa maendeleo ya Kalenga yatakuja tena kwa kasi kubwa," alisema.

Kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea, Dk. Mgimwa alikuwa Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kilichoko eneo la Capripoint mjini Mwanza.

Dk. Mgimwa alishinda kwa kishindo kwa kuwabwaga vigogo kadhaa wa siasa waliokuwa wakichuana naye akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro. Wengine waliogombea katika kura za maoni ni pamoja na Hafsa (Myinga) Mtasiwa ambaye anatoka katika familia ya Mkwawa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo mwaka 2000 hadi 2005, George Mlawa.       

HOMA YA PAMBANO LA WATANI WA JADI YAPAMBA MOTO

HOMA ya ule mpambano wa soka wa watani wa jadi, Simba na Yanga, unaotarajiwa kupigwa majira ya saa 10 alasiri katika dimba la Uwanja wa CCM Kirumba, mjini Mwanza, inazidi kupamba moto.

Kama ilivyo ada unapowadia wakati wa watani wa jadi kupambana, kumekuwa na tambo, vibweka na visingizio kibao kutoka pande zote mbili.

Tangu kuanza kwa wiki hii, Yanga ndio wameonekana kulikamia zaidi pambano hili ambapo Makamu Mwenyekiti wake, Seneta Davis Mosha, amekuwa akisema kuwa Mnyama lazima auawe jijini Mwanza. Jana alikaririwa akisema kikosi chake kiko vizuri tayari kwa pambano la leo.

Wakati Seneta Mosha akitamba, Simba wamedai kuwa kuna njama za kuwahujumu ili wafungwe. Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo, alisema jana kuwa wamepigwa virungu na polisi kwenye uwanja wa Kirumba walipokuwa wakianza maandalizi ya kuuza tiketi kwa ajili ya mpambano huo.

Naye Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, amesema wachezaji wake kadhaa ni majeruhi lakini akasema hiyo haimaanishi kuwa anakubali kushindwa bali ni lazima wafanye kweli katika uwanja wa Kirumba na kuibuka na pointi zote tatu.

Hivyo ni vijimambo vya mpambano wa watani wa jadi ambao unatarajiwa kupigwa saa chache zijazo katika uwanja wa CCM Kirumba katika jiji maarufu kama Rock City.

Dakika 90 za mpambano huo ndizo zitakazoeleza ukweli juu ya nani atatoka mbabe dhidi ya mwenzake. Kila la heri wote.  

MESSIAH CATTERING SERVICES

Messiah Catering Services
For all Locations, For All Occasions
P.O. Box 20811 DAR ES SALAAM Tel: +255 366 792, +255 715 366792  



MENU FOR MEETINGS/SEMINARS/WORKSHOPS

  1. SAMOSA                          8. BEEF KEBAB                 15. POTATO CRIPS
  2. KITUMBUA                       9. FISH FINGER                16. CASHEWNUTS
  3. CAKE                               10. CHICKEN SANDWICH  17. SPICED CHICKEN
  4. MEAT                              11. BEEF SANDWICH        18. CROISANTS
  5. BEEF SAUSAGE ROLL        12. EGG SANDWICH                   19. DOUGHNUTS
  6. BISCUITS                        13. TOMATO SANDWICH 20. BRIOCH
  7. CHICKEN KEBAB               14. CHOCOLATE CAKE     21.CHICKEN DRUMSTICK

PRICE:        TEA/COFFFEE/HOT WATER
                   WITH 2 ITEMS TSHS. 3,500/= PER HEAD-VAT EXCLUDED
                   WITH 3 ITEMS TSHS. 4,500/= PER HEAD-VAT EXCLUDED

COCKTAIL SNACKS MENU

  1. CASHENNUTS                            13. BEEF SAUSAGE ROLL
  2. SAMOSA                                   14. GOAT MEAT
  3. FISH FINGER                             15. CHICKEN LIVER
  4. MEAT BALL                               16. STUFFED EGG
  5. FRIED CHICKEN                         17. CHEESE WITH PINEAPPLE
  6. SPICED CHICKEN                       18. CHICKEN CANAPE
  7. MINI PIZA                                 19. SAUSAGE
  8. VEGETABLE SPRING ROLL          20. CHICKEN DURMSTICKS
  9. VEGETABLE DIPS                       21. TARTARE SAUCE
  10. POTATO CRIPS                         22. MAYONNAISE SAUCE
  11. BEEF KEBAB                               23. TOMATO SAUCE
  12. CHICKEN KEBAB                        24. CHILLY SAUCE

PRICE: 6 ITEMS WITH SAUCE TSHS. 10,000/= PER HEAD EXCLUDING VAT

LUNCH OR DINNER
1.       FRIED CHICKEN      2.  BRAISED BEEF    3.      FISH CUBES MASALLA
4.       PARSLEY POTATOES/VEGETABLE RICE/PLANTAIN
5.       TOMATO CONCASSE/SEASONAL VEGETABLES
6.       SELECTION OF SALADS & DRESSING
7.       VARIETY OF DESSERT

PRICE: TSHS. 10,000/=          PER HEAD EXCLUDING VAT

“ALL PRICES ARE NEGOTIABLE DEPENDING ON THE NATURE OF THE EVENT”